Monday, September 19, 2016

MARAIS WA EAC WACHANGIA TETEMEKO LA ARDHI KAGERA

RAIS John Magufuli amepokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na tetemoko la ardhi lililotokea katika mkoa wa Kagera na mikoa jirani ya Mwanza, Geita na Kigoma kutoka kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo ya maafa na michango kwa ajili ya waathirika wa maafa hayo, Rais Magufuli aliwashukuru wote waliojitoa kusaidia waathirika akiwataja marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuwa wamempigia simu za kumpa pole na tayari wametoa misaada yao.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa Dar es Salaam jana ilisema pamoja na kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli alipokea mchango wa fedha taslimu Dola za Kimarekani 200,000 sawa na takribani Sh milioni 437 kutoka kwa Rais Museveni. Pia Rais Magufuli alipokea taarifa ya mchango wa mabati, blangeti na magodoro vyenye thamani ya Sh milioni 115 kutoka kwa Rais Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Pia alizishukuru nchi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara, watumishi wa umma na watu binafsi waliochangia na kusema michango hiyo ina umuhimu mkubwa katika kukabiliana na athari za maafa haya.

Alitoa wito kwa Watanzania na wote walioguswa na maafa hayo kuendelea kutoa misaada kwa waathirika kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, huku akionya na kuvitaka vyombo vya dola kuwafuatilia watu wanaotaka kutumia maafa haya kukusanya michango kwa lengo la kujinufaisha.