Rais DK. John Pombe Magufuli leo amezindua mpango mkakati wa
kupunguza uharifu nchini huku akilitaka jeshi la polisi kuwasaka kwa udi
na uvumba majambazi nchini kote na kisha kuwachukulia hatua stahiki.
Akizindua mpango huo Rais Dk, Magufuli amesema mpango huo wa miaka
mitatu ambao utaanza kutekelezwa katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni
Julai Mosi, utafanikiwa tu endapo wananchi watashirikiana kikamilifu na
jeshi la polisi , huku akimtaka mkuu wa jeshi la polisi nchini Ernest
Mangu kuhakikisha analisafisha jeshi lake kwa kuwachukulia hatua ikiwemo
kuwafukuza askari wote watakaobainika wanakwenda kinyume na maadili ya
kazi zao.
Wakizungumza katika uzinduzi wa mpango huo ambao lengo lake kuu ni
kukomesha uhalifu nchini ,wafadhili wakuu wa mpango huo wakiwemo benki
ya CRDB ambao wametoa zaidi ya shilingi milioni 320 kujenga kituo cha
kisasa cha mawasiliano pamoja na benki ya NMB ambao nao pia wamejenga
vituo vya polisi viwili vinavyohama , wamesema ulinzi na usalama ni
jukumu la kila mwananchi na kwamba bila usalama na amani hakuna shughuli
yoyote ya kijamii na kiuchumi inayoweza kuendelea.
Awali Rais Magufuli alizindua kituo cha kisasa cha mawasiliano
kilichopo kituo kikuu cha polisi kanda maalum ya Dar es salaam ambapo
akiwa katika viwanja vya biafra alitembelea mabanda mbalimbali ya polisi
ili kujifunza zaidi juu ya mpango huo wa kuboresha usalama wa raia.