MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza wakuu wa mikoa ya Geita,
Arusha na Kagera kuhakikisha wanaondoa mifugo itokayo nje ya nchi
pamoja na kuwaondoa wanachi waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa
(Tanapa) ifikapo Juni 30 mwaka huu.
Aidha ameagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha
wanatenga maeneo maalumu kwa ajili ya mifugo inayotolewa ndani ya
hifadhi na kupunguza mgogoro kwa wananchi wengine.
Samia alitoa maagizo hayo jana jijini hapa, wakati alipokuwa
akikabidhi hundi ya thamani ya Sh bilioni moja kwa wakuu wa mikoa 19
inayozunguka hifadhi za taifa (Tanapa) kwa ajili ya kununua madawati.
Alisema, wakuu wa mikoa wakizembea kutekeleza uondoaji mifugo ndani ya
hifadhi za taifa serikali itawawajibisha.
Alisema waliohifadhi mifugo ndani ya hifadhi hiyo waondoke na mifugo
yao hadi Juni 30 mwaka huu kwani mkoa wa Kagera una ng’ombe milioni
mbili wanaotoka nje ya nchi, na mikoa ya Arusha na Geita ina ng’ombe
milioni tatu kutoka nje ya nchi.
Akizungumzia kuhusu kukabidhi madawati 16,500 katika wilaya zote 55
zilizopo kwenye mikoa 19 nchini, Samia aliipongeza Tanapa kwa kusaidia
elimu nchini kwani baada ya serikali ilipotangaza kuwa elimu bure
wanafunzi wengi wamejitokeza huku kukiwa na changamoto ya madawati Samia
alisema, kutokana na msaada huo wanafunzi wataondokana na adha ya kukaa
chini na kuumia migongo kwani kila wilaya itapata madawati 300 huku
wanafunzi 49,500 wakiwa wanakaa kwenye madawati na kuongeza usikivu
zaidi.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema
Tanapa wanatambua mchango wa elimu ndio maana wametoa msaada huo kwa
mikoa 19 inayopakana na hifadhi za taifa.
Mkurugenzi wa Tanapa, Allan Kijazi alisema Tanapa itaendelea
kushirikiana na serikali katika sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha
wanafunzi wanasoma kwa bidii pamoja na kujua jinsi ya kuhifadhi
maliasili za Taifa.
Akitoa salamu za shukrani kwa Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Said Meck Sadiki aliishukuru Tanapa kwa kutoa madawati kwa
wakuu wa mikoa na kusema kuwa, mkoa wa Kilimanjaro umepiga marufuku
usafirishaji wanyama pori kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA) kuanzia jana.