Mkuu wa wilaya ya Arusha Mjini, Fadhili Nkurlu
Tani 45 za sukari zilizobainika kufichwa katika ghala la mfanyabiashara Karimu Dakiki wa jijini Arusha zimegawiwa kwa watendaji wa kata 25 za jiji la Arusha ili wazisambaze kwa wananchi katika kata hizo.
Zoezi hilo la kugawa sukari kwa watendaji wa kata hizo limesimamiwa na Mkuu wa wilaya ya Arusha Mjini, Fadhili Nkurlu.
Nkurlu amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la serikali la kukabilina na hujuma ya baadhi ya wafanyabiashara wanaosababisha uhaba wa sukari kwa maslahi yao binafsi.
Kwa upande wake Kaimu Afisa biashara wa jiji la Arusha, Godfrey Edward amesema bado kuna uhaba wa sukari hivyo bidhaa hiyo iliyogawawiwa itapunguza makali ya uhaba.
Uongozi wa mkoa wa Arusha umeendelea kuwaonya wafanyabiashara wasio waaminifu kuacha kuficha sukari kwa lengo la kuwalangua wananchi kwa kuwauzia kwa bei ya juu.
Sechelela Kongola
08 May 2016