Monday, May 2, 2016

Trump asema Uchina “inaibaka” Marekani


Trump
Mgombea mkuu wa chama cha Republican Donald Trump ameshutumu Uchina na kusema imekuwa “ikiibaka” Marekani kupitia s
era zake za kibiashara.
Ameambia watu waliohudhuria mkutano wa kisiasa Indiana kwamba Uchina imekuwa ikitekeleza “wizi mkubwa zaidi kuwani kutekelezwa katika historia ya dunia.”
Bw Trump, mfanyabiashara tajiri kutoka New York, amekuwa akiituhumu Uchina kwa kuchezea sarafu yake ili kuwa na ushindani wa kibiashara duniani inapouza bidhaa nje ya nchi.
Hilo, amesema, limeathiri sana wafanyabiashara na wafanyakazi wa Marekani.
“Hatuwezi kuruhusu Uchina iendelee kuibaka nchi yetu, na hilo ndilo tunafanya (kwa wakati huu),” alisema mkutanoni Jumapili.
"Tutabadilisha mambo, na tuna uwezo, msisahau. Tuna nguvu sana dhidi ya Uchina.”
Katika manifesto yake ya kampeni, Bw Trump ameahidi kufanikisha mkataba bora wa kibiashara baina ya Uchina na Marekani ambao utawezesha “wafanyabiashara na wafanyakazi kutoka Marekani kuweza kushindana”.
Ametaja malengo manne ambayo yanahusisha kutangaza Uchina kuwa taifa linalochezea sarafu yake na kusitisha utoaji wa nafuu za wafanyabiashara wanaouza bidhaa nje ya nchi ambazo anasema ni haramu.
Aidha, anaitaka Uchina kufikisha kikomo mfumo duni wa masharti ya leba na uhifadhi wa mazingira.